top of page

Kutafuta Waliopotea

Kuwaandaa Watakatifu

Kuandaa Kanisa

Anchor 1
god 3.jpg

Kuhusu mimi

Kwa majina ninaitwa Japhet Mkondya, mwalimu wa Neno la Mungu, mwandishi, mwanamuziki na rafiki wa Roho Mtakatifu. Ni baraka sana kuitwa katika misheni kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Shauku yangu ni kuona wengi wakimpokea Yesu ili awe mwokozi wao binafsi na kuishi maisha ya utukufu ambayo Mungu alikusudia kanisa lake liishi. Kwa neema ya Mungu, nilijitolea kumtumikia Mungu kupitia kufundisha na kuhubiri neno la Mungu katika sehemu mbalimbali duniani. Kupitia safari hii pamoja na Yesu, imekuza shauku kubwa ndani yangu ya kuliona kanisa la Yesu Kristo likitembea katika njia sawa na jinsi Kanisa la kwanza lilivyotembea katika Kitabu cha Matendo ya mitume. Hii imenipelekea kuendelea kufanya makusanyiko mbalimbali ya maombi, semina za neno la Mungu na harakati za uinjilisti ndani na nje ya africa. Kwa hiyo, ninaongoza kambi mbalimbali za maombi duniani kote nikifanya kazi na watu ambao wamejitolea kweli kweli na wana shauku ya kuona Injili ya ufalme wa Mungu ikiwafikia wengi. Ninaamini katika Mungu ambaye anapenda kila mtu na kwamba bado anawaita wote watubu (Mt 4:17) ili wapate uzima wa milele unaopatikana katika Kristo Yesu (Yohana 3:16). Nilivyokabidhiwa na Baba wa Mbinguni kuongoza huduma hii; Ni imani yangu kuwa kila alichoanzisha Mungu atakidumisha milele.

8ce7a1_06087b39a22645909cac26f1d206f4af_mv2.webp

Kuhusu sisi

post-18-1170x658.jpg

Huduma inahusu nini

Sisi ni huduma isiyo fungamana na dhehebu lolote, wafanyakazi wa misheni wa siku za mwisho, ambao lengo lao ni kufikia ulimwengu kwa Injili ya Yesu Kristo, na kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Kama vile tulivyopewa agizo kuu (Mathayo 28:16-20, Marko 15:16-17), kazi yetu ni kuitikia na kuhakikisha tunafanya kazi yake yeye aliyetutuma kungali bado mchana. Huduma yetu inafafanuliwa kupitia maeneo makuu matatu ambayo ni kutafuta waliopotea, kuandaa watakatifu na kuandaa kanisa kwa ajili ya ujio wa pili wa Yesu Kristo. Tulipoanza kutembea katika huduma hii pamoja na Bwana tumeona wengi wakija kwa Kristo, watu waliponywa na huu ndio uthibitisho wa maneno kutoka kwa mwokozi wetu Yesu Kristo aliposema: “Mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata mwisho. wa dahari” (Mathayo 28:20b).

WhatsApp Image 2022-10-26 at 16.49.21.jpg

Huduma inafanya nini

Tangu mwaka 2014 Tumejitoa kwa Bwana Yesu kwa kuendesha mikutano ya injiri barani Afrika. Tulianza Tanzania kwa kuandaa semina za ndani. Baadaye, tulikwenda Ulaya na kulenga kufikia nchi za Amerika Kusini; kwa lengo la kuwatayarisha watakatifu kwa ajili ya kazi ya huduma. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu, Tumekuwa tukitoa nyenzo za Injili kama vile Biblia, Vitabu kwa wamisionari kote ulimwenguni, Vinavyoweza kuwasaidia wakati wa mahubiri. Msukumo wetu ni kuona watu wakisoma na kuishi Neno la Mungu kwa sababu tunajua kwamba Wakristo wachache sana wanaweza kupata Neno la Mungu. Lengo letu ni kuwafikia wengi kwa kadri Mungu atakavyo tusaidia , Tuko hapa kusema wazi kwamba huduma yetu inamtegemea Roho Mtakatifu asilimia mia moja. Tunafuata anayosema, na kufanya yale anayotuambia tufanye.Tunaamini kuwa Neema ya Mungu imemiminwa kwa kila mtu kwa njia ya Kristo Yesu na kila mtu anatakiwa kusikia Habari Njema hizi. Kwa hiyo tunaitwa kwa ajili ya wasiofikiwa, wasiopendwa na wale ambao wamesahauliwa. tunakukaribisha sana kwa kushirikiana nasi, ili kwa pamoja tuweze kuwafikia wengi kadiri Mungu atuwezeshavyo. Bwana Yesu Kristo akubariki.

Amini Yetu

Tunamwamini Mungu.

Mungu ni mwenyezi na ni mmoja tu. Hakuna Mungu mwingine ila yeye.

Tunaamini kwamba Mungu anaonekana katika nafsi tatu. 

 

Tunamwamini Mungu Baba.

Mungu ndiye muumbaji na hapo mwanzo aliziumba mbingu na nchi na vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. 

 

Tunamwamini Yesu Kristo.

Yesu ni Mungu aliyefanyika mwili, Mungu akawa mwanadamu ndani ya Yesu. Alichukuliwa mimba na Roho Mtakatifu na kuzaliwa na Bikira Maria. Yeye ni mwanadamu kamili na Mungu kamili. Aliishi bila dhambi na alikufa kwa ajili ya dhambi zetu msalabani. Lakini alishinda kifo na akafufuka kutoka kwa wafu. Yeye ndiye mwokozi wetu pekee na njia pekee ya kwenda kwa baba. Atarudi na kusimamisha ufalme wake wa milele. 

 

Tunamwamini Roho Mtakatifu. 

Anakaa ndani ya kila Mkristo wa kweli na anasadiki dhambi zetu.

Mungu ametupa Roho Mtakatifu ambaye hutufundisha na kutuongoza katika utakatifu. Anatusaidia katika udhaifu wetu na kutupa nguvu kwa maisha yetu katika Kristo. Anatuombea kwa maombi. 

 

Tunaamini katika Biblia.

Ni neno pekee la Mungu na ni kweli kabisa. Imevuviwa na Roho Mtakatifu na haina makosa. Tunaamini kwamba Biblia ndiyo mamlaka ya mwisho ambayo inatuonyesha jinsi Mungu alivyo na jinsi tulivyo na jinsi tunavyopaswa kuwa. 

 

Tunaamini katika Injili. 

Mwanadamu ameumbwa na Mungu na ameumbwa kuwa na uhusiano na Mungu lakini sisi tumemkosea Mungu. Dhambi inatupeleka katika mauti ambayo ina maana ya kutengwa kabisa na Mungu na kupotea. Tunaamini kwamba Yesu alikuja duniani kurejesha uhusiano huu. Alitangaza neno la Mungu na mwanzo mpya na agano jipya. Tunaamini kwamba alikufa msalabani na kwamba tunapata wokovu kupitia kwake. Ni kwa neema tu na kwa damu ya Yesu. Kila mtu anayeamini Injili lazima atubu dhambi zake ili maisha mapya yaweze kusimikwa ndani yao, na anayemruhusu Yesu kuja katika maisha yao, azaliwe mara ya pili na ni mtoto wa Mungu. Watoto wa Mungu wana wokovu kupitia Yesu na wataishi milele mbinguni. 

Tunaamini katika ushirika wa watakatifu.

Katika kanisa takatifu la Yesu Kristo ambalo ni umoja katika ulimwengu wote. Tunaamini kwamba Wakristo wameitwa kutangaza Injili na kwamba Wakristo wanahimizana katika imani. Tunaamini kwamba tunafuata utakatifu na kwamba kila mtu amepewa karama zake mwenyewe ambazo anapaswa kumtukuza Mungu mbinguni na kuwatumikia wanadamu, hasa Wakristo.

 

Tunaamini katika Misheni.

Tunapopokea neema na uzima wa milele, tunaamini kwamba kila mtu anahitaji kusikia Habari Njema hii. Kwa kuonyesha imani yetu kwa bidii na kwa kuishi neno la Mungu, tunabeba utume ambao Yesu ametupa katika Mathayo 28:16-20 (agizo kuu) na kueneza Injili kwa mataifa yote.

®© Hakimiliki™
© 2022 na Japhet Mkondya Ministries. Inaendeshwa na UniPegasus Infotech Solutions.
  • Instagram
  • Facebook
  • YouTube
bottom of page